Deuteronomy 21:1-9

Upatanisho Kuhusu Mauaji

1 aKama mtu akikutwa ameuawa, naye amelala kwenye shamba katika nchi ambayo Bwana Mungu wenu anawapa kuimiliki, wala haijulikani ni nani aliyemuua, 2wazee wenu na waamuzi watatoka na kupima umbali kutoka maiti alipolala mpaka kwenye miji ya jirani. 3 bKisha wazee wa ule mji ulio karibu zaidi na yule maiti watamchukua mtamba ambaye hajapata kufanyishwa kazi na ambaye hajafungwa nira, 4na kumpeleka kwenye bonde ambalo halijapata kulimwa au kupandwa mazao na ambapo kuna chemchemi itiririkayo. Huko kwenye hilo bonde, wazee watamvunja yule mtamba shingo. 5 cMakuhani, hao wana wa Lawi, watasogea mbele, kwa kuwa Bwana Mungu wenu, amewachagua kuhudumu na kutoa baraka katika jina la Bwana, na kuamua mashauri yote ya mabishano na mashambulio. 6 d , eNdipo wazee wote wa mji ulio karibu zaidi na huyo maiti watanawa mikono yao juu ya huyo mtamba ambaye shingo yake imevunjwa huko kwenye bonde, 7 fnao watatangaza: “Mikono yetu haikumwaga damu hii, wala macho yetu hayakuona likifanyika. 8 gEe Bwana, ukubali upatanisho kwa watu wako Israeli, ambao umewakomboa, wala usiwahesabie watu wako hatia ya damu ya mtu asiyekuwa na hatia.” Nayo damu iliyomwagika itakuwa imefanyiwa upatanisho. 9 hHivyo mtakuwa mmejitakasa wenyewe kutoka hatia ya kumwaga damu isiyokuwa na hatia, kwa kuwa mmefanya lile lililo sawa mbele za macho ya Bwana.

Copyright information for SwhNEN